HABARI Mahakama Kuu ya Uhispania imetuhumu kufanya uasi, rais wa zamani wa jimbo lenye mamlaka ya ndani ya Catalonia Carles Puigdemont aliyeko uhamishoni nchini Ubelgiji na washirika wake 12 wanaounga mkono kujitangazia uhuru kwa jimbo hilo. Tuhuma hizo ni hatua nyingine kuelekea kuwafungulia mashtaka wanaharakati hao ambapo iwapo watapatikana na hatia wanaweza kukabiliwa na kifungo cha miaka 30 jela. Wengine wanaokabiliwa na tuhuma hizo ni aliyekuwa naibu wa Puigdemont, Oriol Junqueras, wanaharakati wa mashirika ya kiraia Jordi Sanchez na Jordi Cuixart, pamoja na aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani wa Catalonia, Joaquim Forn. Maafisa hawa wanne wamekuwa wakishikiliwa kizuizini kwa miezi wakisubiri kufikishwa mahakamani. Aliyekuwa spika wa bunge la jimbo la Catalonia Carme Forcadell pia ni miongoni mwa washtakiwa. Baadaye mahakama hiyo itaamua ikiwa aliyegombea urais wa jimbo hilo Jordi Turull pia anapaswa kufunguliwa mashtaka. 

Maoni

Machapisho Maarufu