HABARI Polisi ya Ufaransa imemuua kwa risasi mtu mwenye silaha aliyekuwa akiwashika mateka watu katika duka moja kwenye mji mdogo wa Trebes ulio kusini mwa nchi hiyo. Mbali na mtekaji nyara huyo, watu wengine watatu wameuliwa katika tukio hilo ambalo serikali ya Ufaransa inalichukulia kuwa la kigaidi. Wizara ya mambo ya ndani ya Ufaransa imesema wawili wameuawa ndani ya duka lililotekwa, na mwingine alipigwa risasi kichwani na mshambuliaji huyo katika mji jirani wa Carcassonne. Kituo cha televisheni cha BFM kimeripoti kwamba mtekaji nyara huyo alikuwa amedai kuwa mfuasi wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu - IS, na kwamba alikuwa akitoa masharti ya kuachiwa kwa mshukiwa mkuu wa mashambulizi ya kigaidi ya mwaka 2015 yaliyoua watu 130 mjini Paris, Salah Abdesalam. Chanzo kilicho karibu na upelelezi kimeliambia shirika la habari la Reuters, kwamba polisi wawili wamejeruhiwa kuhusiana na tukio hilo. 

Maoni

Machapisho Maarufu